
KIONGOZI wa Kanisa Katoliki duniani PAPA Francis ameaga dunia leo katika Jumatatu ya Pasaka akiwa na umri wa miaka 88. Kwa mujibu wa Vatican, Papa amefariki asubuhi ya saa 1.35 za Italia. Kwa mujibu wa historia na mapokeo, hadi Papa Francis anaaga dunia, Kanisa Katoliki limeongozwa na mapapa 266.
Kardinali Farrell ametangaza kwa huzuni kifo cha Papa Francis, kwa maneno haya:
“Ndugu wapendwa, kwa huzuni kuu ninapaswa kutangaza kifo cha Baba Mtakatifu wetu Francis. Saa 1:35 asubuhi hii, Askofu wa Roma, Francis, amerudi nyumbani kwa Baba. Maisha yake yote yalitolewa kwa ajili ya kumtumikia Bwana na Kanisa lake. Alitufundisha kuishi maadili ya Injili kwa uaminifu, ujasiri na upendo wa wote, hasa kwa maskini na waliotengwa. Kwa shukrani kubwa, kwa mfano wake kama mfuasi wa kweli wa Bwana Yesu, tunakabidhi roho ya Papa Francis kwa upendo wa huruma usio na mipaka wa Mungu katika Utatu Mtakatifu.”
Mapokeo ya Kanisa humtambua Mtume Petro kama Papa wa kwanza aliyeongoza Kanisa kwa miaka 34 tangu mwaka 30 hadi 64, akifuatiwa na Papa Linus (64-76), Papa Anacletus (76-88) na wengine 262 kabla ya Francis. Papa Francis, ambaye jina lake halisi ni Jorge Mario Bergoglio, alichaguliwa kuwa Papa tarehe 13 Machi 2013 kuchukua nafasi ya Papa Benedicto XVI (2005-2013).
Wiki kadhaa zilizopita Papa Francis alilazwa hospitalini kutokana na “maambukizi” aliyopata. Baada ya kupata nafuu, aliruhusiwa. Jana, katika Sikukuu ya Pasaka, Papa Francis alijitokeza katika St. Peter’s Square kuwatakia Wakristo wote Pasaka Njema. Viongozi kadhaa duniani wanaendelea kutoa Salaam za rambirambi kwa Vatican na Kanisa Katoliki duniani.
Katika andiko hili, Padre Patrick Coelestine Tibangayuka, Gombera wa Seminari Kuu Ntungamo, Jimbo Katoliki la Bukoba, anaeleza utaratibu wa kawaida unaopaswa kufuatwa na Kanisa Katoliki kupata mrithi wa Papa, kifo kinapotokea.

……………………………………………………………………………..
MADA YENYEWE: Ili kuelewa vizuri utaratibu wa kufuata pale Baba mtakatifu anapokuwa ameaga dunia waweza kusoma nyaraka zifuatazo, mintarafu utaratibu wa kufuata baada ya kifo cha Baba Mtakatifu:
(ii) Maelekezo mintarafu taratibu za kufuata baada kifo cha Papa. Waraka huu ulitolewa na baba Mtakatifu Paulo VI mnamo mwaka 1975.
(ii) Universi Dominici Gregis (yaani, Mchungaji wa kundi lote la Bwana). Waraka huu ulitolewa na Baba Mtakatifu Yohane Paulo wa Pili.
(iii) Normas Nonnulas (yaani, Baadhi ya Kanuni). Waraka huu ulitolewa na Baba Mtakatifu Benedikto XVI mnamo mwaka 2013.
Kwa ufupi waraka tajwa wa Baba Mtakatifu Paulo VI ulitamka yafuatyo:
Camerlengo, yaani, msimamizi mkuu wa nyumba ya kitume [apostolic palace] na mali za kitume [apostolic heritage], wa Kanisa Takatifu la Roma [hapa inamaanisha Dayosisi ya Roma] atathibitisha kifo cha Papa.
Itampasa Camerlengo kumjulisha Kardinali Wakili kwa ajili ya Jiji la Roma (Cardinal Vicar for the City of Roma). Itambidi Kardinali Wakili kuwajulisha waamini wa Dayosisi ya Roma. NB: Ikumbukwe, kwa kawaida Baba Mtakatifu, kama askofu wa Dayosisi ya Roma, anakuwa na Mawakili (Vicars general) wawili: Kardinali Wakili kwa ajili ya Jiji la Roma (Cardinal Vicar for the City of Rome); na Kardinali Wakili kwa ajili ya Jiji-Dola ya Vatikano (Cardinal Vicar for the Vatican City State).
Itambidi Camerlengo kufunga kwa ‘seal’ maalum vyumba vyote vya kipapa.

Hatua za mazishi zitafanyika na kutangazwa.
Makardinali watakusanyika kwa mkutano maalumu wa faragha (conclave) kwa lengo la kumchagua Papa.
Hakuna Kardinali mwenye umri zaidi ya miaka 80 atashiriki mkutano (conclave) wa kumchagua Papa.
Kwa ufupi, waraka tajwa hapo juu, yaani, Universi Dominici Gregis wa Baba Mtakatifu Yohane Paulo II ulisema yafuatayo mintarafu kiti cha Kitume kinapokuwa wazi:
Kiti cha Kitume kinapokuwa wazi, makardinali hatakuwa na uwezo (jurisdiction) juu ya shughuli zote zilizomhusu Baba Mtakatifu wakati wa uhai wake au yaliyohusu ofisi yake kama Papa. Mambo hayo yote yatamsubiri Papa atakayemrithi.
Wakati kiti cha kitume kinapokuwa wazi, utawala wa Kanisa unakuwa mikononi mwa Baraza la Makardinali kwa mambo yale tu ambayo hayawezi kuhairishwa; na kwa mambo yanayohusu maandalizi ya kumchagua Papa.
Baraza la Makardinali hawawezi kufanya mabadiriko yoyote kuhusu haki za Kiti cha Kitume (Apostolic see) na za Kanisa la Roma (Dayosisi ya Roma), bali kwa pamoja watalinda haki hizo.
Wakati Kiti cha Kitume kinapokuwa wazi, sheria zilizotungwa na Papa haziwezi kusahihishwa au kurekebishwa; na hakuna chochote kiwezacho kuongezwa au kuondolewa, na hakuna yeyote anayeweza kupata kibari cha kutozifuata.
Kama kuna jambo halieleweki kuhusu sheria na kanuni yoyote wakati kiti cha kitume kinapokuwa wazi, ni baraza la makardinali lenye uwezo wa kushughulikia mashaka hayo na kutoa tafsiri sahii ya jambo/mambo hayo. Hili hili lifanyike inalazimu sehemu kubwa ya makardinali wawepo (simple majority).
Kama kuna jambo litajitokeza ambalo haliwezi kuhairishwa, Baraza la Makardinali litashughulikia jambo hilo na kutoa jibu kwa mjibu wa kauli ya makardinali walio wengi (voice of the simple majority).
Kwa ufupi, waraka tajwa (Normas Nonnulas) wa Baba Mtakatifu Benedict XVI ulisema yafuatayo kama nyongeza kwa nyaraka tajwa hapo juu, hasa waraka Universi Dominici Gregis :
Makardinali wanatengewa eneo ndani ya jiji la Vatikano pasipo kuwasiliana na watu wanje wakati wote wa mkutano wa faragha (conclave).

Theluthi mbili kuongeza kura moja zitahitajika kumtangaza Papa.
Baba Mtakatifu aliyechaguliwa atavaa kanzu nyeupe akiwa ndani ya Chumba cha Machozi kabla hajarudi kwenye chumba cha faragha (conclave).
Ni Imani yangu dondoo hizi zimetoa mwanga na kuondoa dukuduku juu ya taratibu za kufuata kama Baba Mtakatifu amekufa au kama kiti cha papa ki wazi kwa sababu nyingine.
Ikumbukwe pia kuwa Camerlengo huthibitisha kifo cha Papa mbele ya Mliturjia Mkuu wa Kipapa (Papal Master of Ceremonies) na mbele ya wajumbe wengine wakaao katika nyumba ya kipapa.
Vile vile picha au filmu za Papa iwe katika kitanda cha kifo au baada ya kifo haziruhusiwi kabisa.
Lakini pia, ikiwa Baba Mtakatifu alikuwa ameandika wosia na kumteua mwosia (executor of the will), mwosia huyo atatoa taarifa juu ya wosia huo kwa Papa mpya tu.
Kuhusu mazishi ya Papa: Baada ya kifo cha Papa kunakuwepo na siku kenda (9) za maombolezo, na mazishi hufanyika kati ya siku ya 4 na ya 6 baada ya kifo isipokuwa kama kuna sababu maalumu.
Kama Papa hakusema vinginevyo wakati wa uhai wake, kwa kawaida mazishi ya Papa hufanyika ndani ya Basilica ya Mt. Petro, ambapo mwili wa Papa utawekwa kwa lengo la kutolewa heshima.